Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Hafla ya uzinduzi wa filamu ya “Wakili”, inayosimulia historia ya mapambano ya Lebanon na nafasi muhimu ya Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Isa Tabatabaei, mwakilishi wa Imam Khomeini (r.a) na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Lebanon, ilifanyika siku ya Jumanne katika Husayniyya ya Sanaa.
Katika hafla hiyo, Muhammad Mahdi Shariatmadar - aliyewahi kuwa balozi wa kitamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon - alimtaja mwanachuoni huyu shujaa kuwa ni mtu wa kipekee, aliyejeruhiwa na adui lakini ndiye aliyeweka msingi wa njia ya mapambano.
Shariatmadar, katika utangulizi wa hotuba yake, aliwashukuru Husayniyya ya Sanaa na Tamasha la Ammar kwa kuandaa hafla hiyo, akisema:
“Ninawashukuru kwa mara ya pili kumheshimu mtu huyu wa kipekee. Mara ya kwanza alitambuliwa katika Tamasha la Ammar, na sasa ni mara ya pili tunapomkumbuka mtu aliyeumizwa – si tu na adui, bali pia na magumu na wasiwasi wa njia ya jihadi na mapambano yake.”
Akizungumza kuhusu nafasi ya Sayyid Isa Tabatabaei, alisema:
“Kama kazi inavyodhihirisha ubora wa mtunzi wake, ndivyo mafanikio yake yanavyoweza kutufahamisha undani wa utu wake. Ingawa filamu ya Wakili ni kazi yenye thamani, lakini kwa maoni yangu haikuweza kuakisi kwa ukamilifu pande zote za uhai wa Tabatabaei, kwani yeye ni zaidi ya filamu moja ya kumbukumbu.”
Shariatmadar alielezea historia ya mapambano ya Lebanon akisema:
“Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kulikuwepo wanachuoni watatu wakubwa - Imam Musa Sadr, Sayyid Muhammad Hussein Fadlallah, na Sheikh Muhammad Mahdi Shamsuddin - waliokuwa waanzilishi wa harakati ya mapambano nchini Lebanon. Baada ya Mapinduzi, wanazuoni na wasomi kutoka Iran kama Imam Musa Sadr, Shahid Mustafa Chamran, Ayatullah Akhtari, marehemu Mohtashamipour na marehemu Hussein Sheikh al-Islam walichukua nafasi muhimu katika kuendeleza njia hiyo. Hata hivyo, miongoni mwa wote hawa, Sayyid Isa Tabatabaei alikuwa na nafasi ya kipekee.”
Aliongeza kusema:
“Ikiwa Imam Musa Sadr alikuwa mwanzilishi wa taasisi za kijamii na kitamaduni za Waislamu wa Kishia nchini Lebanon, basi Sayyid Isa Tabatabaei ndiye aliyepuliza roho ya mapambano ndani ya jamii ya Kishia na kuifanya kuwa sehemu ya utambulisho wao. Kutokana na juhudi zake, ndipo mapambano ya kisasa ya Lebanon yalipozaliwa – mapambano ambayo baadaye yalifikia kilele chake katika kuunga mkono malengo ya Palestina.”
Shariatmadar pia aligusia maisha yenye changamoto ya Tabatabaei, akisema:
“Sayyid Isa alizaliwa akiwa yatima, akatengana na mama yake utotoni, na akaishi maisha ya uhamaji kwa miaka mingi. Kutoka Najaf hadi Damghan, Qom na Kermanshah, kisha akaelekea Iraq na Lebanon - alipitia njia yenye milima na mabonde mengi. Lakini kutokana na uhamaji huo, alitokea mtu aliyebadilisha mustakabali wa Waislamu wa Kishia wa Lebanon, harakati ya mapambano ya Kiislamu, na wazo la umoja wa Ummah wa Kiislamu.”
Alisema zaidi:
“Sayyid Isa alisomea dini akiwa Damghan, Qom na Kermanshah, na alivalishwa joho la ualimu na Shahid Ashrafi Isfahani. Aliyakumbuka miaka hiyo kama kipindi bora zaidi cha maisha yake. Huko Kermanshah alikutana na wanaharakati wa Fadā’iyān-e Islam, na kusoma kitabu Kashf al-Asrār cha Imam Khomeini (r.a) kulimfanya awe na uhusiano wa kiroho na fikra za Uwilaya na siasa za Kiislamu.”
Shariatmadar alisisitiza kuwa:
“Yeye ndiye aliyeanzisha karibu taasisi zote za kijamii, kitamaduni, kidini na za huduma za jamii miongoni mwa Waislamu wa Kishia wa Lebanon - kuanzia Kamati ya Misaada (Komite-ye Emdad), Shirika la Mashahidi, Taasisi ya Majeruhi wa Mapambano, Mfuko wa Mikopo ya Kheri, Jihad al-Ujenzi, na Mfuko wa Kowsar, hadi vituo 40 vya kitamaduni vya Imam Khomeini katika miji na vijiji, hospitali ya Rasul A‘zam mjini Beirut, hospitali ya Sheikh Raghib Harb mjini Nabatieh, Hawza ya Imam Khomeini mjini Baalbek, Kaburi la Bibi Khawla (s), Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu, kituo cha televisheni Al-Manar, na shule za misaada. Leo taasisi hizi ndizo nguzo kuu za jamii ya mapambano nchini Lebanon.”
Aliongeza:
“Sayyid Isa alizikabidhi taasisi zote hizi kwa Hizbullah, jambo linalodhihirisha kiwango cha juu cha ikhlasi na kutokuwa na tamaa ya mamlaka au mali. Ni wachache wanaoweza kuachia mafanikio makubwa namna hii bila matarajio yoyote ya faida binafsi.”
Akiendelea, Shariatmadar alielezea upande wa kiroho wa mwanachuoni huyo akisema:
“Safari yake ya kwanza ya Hija aliifanya kwa niyyah ya Bibi Fatimah Zahra (s), na alikuwa na uhusiano wa karibu na Qur’ani Tukufu. Kila siku alikuwa akisoma angalau juzuu mbili, na katika mwezi wa Ramadhani mara nyingine alimaliza Qur’ani kwa siku moja tu.”
Kwa mujibu wa Shariatmadar, Sayyid Hassan Nasrallah amewahi mara nyingi kumsifu Sayyid Isa kwa unyenyekevu na upendo wake mkubwa kwa wananchi wa Lebanon, familia za mashahidi na wapiganaji wa mapambano.
Alisema pia:
“Katika mwisho wa filamu hiyo, swali linaulizwa: je, Israel inaweza kukomesha historia ya mapambano? Jibu langu ni hapana. Maadamu kuna uvamizi, mapambano yataendelea kuwa hai. Mapambano si bunduki na makombora pekee, bali ni roho na ari iliyomo ndani ya watu waumini na wenye uelewa. Hata katika mazungumzo ya sheria za kimataifa, haki ya kujilinda kupitia mapambano imetambuliwa.”
Shariatmadar alihitimisha kwa kusema:
“Sayyid Isa Tabatabaei hakuwa tu mjenzi wa majengo na taasisi, bali alikuwa mjenzi wa utamaduni wa mapambano. Aliamini kwamba tunaweza kusimama imara - na tunapaswa kusimama imara.”
Alihitimisha hotuba yake kwa kunukuu maneno ya Sayyid Hassan Nasrallah:
“Yote tunayoyasema kuhusu Sayyid Isa hayawezi hata kidogo kulipa haki yake. Haki yake juu yetu, juu ya watu na juu ya njia ya mapambano, ni haki kubwa na ya milele.”
Your Comment